Published 2024-06-01 07:37:44 by JKCI
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group kufanya upimaji wa magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyoambukiza kwa wakazi na waumini wa KKKT Kitunda.
Upimaji huo ulioanza jana unafanyika kwa siku tatu katika kambi maalumu ya tiba mkoba ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services katika viwanja vya kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani jimbo la kati Usharika wa Kitunda Relini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Samueli Rweyemamu alisema upimaji huo umefanyika katika eneo la kanisa kuwapa nafasi watu kuonana na mchungaji kwani wapo watu wenye changamoto za familia na maisha zinazowapelekea kupata magonjwa yasiyoambukiza.
“Katika kambi hii tumekuja na daktari bingwa wa saikolojioa kuangalia afya ya akili kwani tatizo la afya ya akili limekuwa kubwa katika jamii, watu wenye tatizo hilo wakirudi kwa mchungaji wakapata huduma za kiroho watakaa vizuri na kuepuka magonjwa ya shinikizo la damu”, alisema Dkt. Rweyemamu
Dkt. Rweyemamu alisema lengo kuu la kambi hiyo ni pamoja na kufikisha huduma katika jamii, kutoa ushauri wa namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na kutoa huduma za matibabu endelevu kwa watu watakaogundulika kuwa na magonjwa yasiyoambukiza.
“Katika kambi hii tutatoa huduma za kuchunguza na kutoa chanjo ya homa ya ini, kuchunguza na kutoa matibabu ya kansa na tezi dumu, kuchunguza na kutoa matibabu ya magonjwa ya sukari, shinikizo la damu na moyo, kuchunguza na kutoa matibabu ya matatizo ya masikio pamoja na kutoa huduma kwa watu wanaohitaji ushauri wa kimwili na kiroho”, alisema Dkt. Rweyemamu
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Eva Wakuganda aliwataka wakazi wa kitunda na maeneo ya jirani kutumia siku tatu za kambi hiyo kuwafikisha watoto kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo.
Dkt. Eva alisema wazazi wakiwa na utaratibu wa kuwafanyia uchunguzi wa afya watoto wao watawasaidia kugundua matatizo ya kiafya mapema na kumpa nafasi mtoto kupata matibabu mapema kwani magonjwa mengi ya moyo kwa watoto yanakuwa na muda wa matibabu na pale muda unapovuka inakuwa ngumu kumtibu mtoto.
“Kuna wakati tunakutana na changamoto za matibabu kwa watoto wenye magonjwa ya moyo kwani unakuta mtoto alihitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo kabla hajafikisha mwaka mmoja lakini kwasababu mzazi hakugundua mapema anamleta mtoto akiwa na zaidi ya mwaka mmoja hivyo kukwamisha baadhi ya matibabu”, alisema Dkt. Eva
Naye Mkuu wa jimbo la kati kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani Mchungani Frank Kimambo aliwataka waumini wa KKKT kuona umuhimu wa kufanya uchungzi wa afya ili washiriki kikamilifu katika kumtumikia Mungu pamoja na kushiriki katika shughuli za kiuchumi na maendeleo kwa kuwa shughuli hizo zinahitaji watu wenye afya.
Mchungaji Kimambo alisema kati ya ibada zote zilizofanyika mwaka huu katika Kanisa la KKKT Usharika wa Kitunda Relini hii imekuwa ibada kubwa kwani waumini na wakazi wa kitunda wameweza kufikiwa na huduma za afya bila gharama hivyo kuushukuru uongozi wa kanisa hilo.
“Nawashukuru madaktari bingwa wa JKCI, Ocean Road, Muhimbili na Hospitali ya Magereza kwa kuacha ofisi zenu na kuja kutuhudumia, Mungu amewapa uwezo kwaajili ya kushughulika na miili hii iliyoumbwa naye, nisadaka kubwa sana mmeitoa kwaajili yetu”, alisema Mchungaji Kimambo
Upimaji huo unafanywa na madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) na Hospitali ya magereza ya Ukonga.