Utalii tiba waongeza idadi ya wagonjwa wanaotibiwa JKCI
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Tuesday, Apr 08, 2025
Upatikanaji wa huduma za Utalii tiba katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) umesaidia kuongeza idadi ya wagonjwa wa nje ya nchi kutoka wagonjwa 316 mwaka 2023 hadi kufikia wagonjwa 689 mwaka 2024 wanaotibiwa na Taasisi hiyo.
Hayo yamesemwa na Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Benjamini wakati wa maadhimisho ya wiki ya Afya Kitaifa inayofanyika katika viwanja vya kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete kilichopo jijini Dodoma.
Dkt. Alex alisema ukilinganisha na miaka ya nyuma kabla ya kuanzishwa kwa kampeni za utalii tiba nchini wagonjwa waliokuwa wanafika JKCI walikuwa kutoka nchi chache tofauti na ambavyo sasa wanapokea wagonjwa kutoka nchi nyingi zaidi.
“Kupitia kampeni ya utalii tiba nchini JKCI sasa tunapokea wagonjwa kutoka nchi za Somalia, Malawi, Kenya, Rwanda, Jamhuri ya Watu wa Comoro, Zambia, Uganda, Msumbiji, Nigeria, Congo, Ethiopia, Burundi, Siera Leone, Zimbabwe na wengine kutoka nje ya Afrika katika nchi za Armenia, China, Ujerumani, India, Uingereza, Ufaransa na Norway”, alisema Dkt. Alex
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa Dodoma waliotembelea banda la JKCI wamesema kuwepo kwa banda la taasisi hiyo katika maonesho hayo kumewapa fursa adhimu ya kujifunza na kuijua vizuri taasisi hiyo.
Wananchi hao wamesema uwekezaji uliofanywa katika sekta ya afya umesaidia kupunguza idadi ya wagonjwa kwenda nje ya nchi kufuata huduma za kibingwa hivyo kuzitumia vizuri hospitali zilizopo nchini.
Mwanada Kimambo alisema huduma za afya nchini ziendane na maendeleo ya sayansi na teknolojia ili utalii tiba unaofanywa na JKCI uendelee kupata wadau wengi kutaka kutibiwa Tanzania.
“Kuna wakati nilisikia wataalamu kutoka Burkina Faso wamekuja JKCI kujifunza, kwakweli sikuamini kama sasa Tanzania tupo kwenye kiwango cha juu katika huduma za matibabu ya moyo hadi mataifa mengine wanakuja kujifunza kwetu”, alisema Mwanada
Naye Ibrahimu Mwilo alisema serikali ya awamu ya sita imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya afya kwani sasa wananchi wanapata huduma za afya kwa urahisi kutokana na huduma hizo kupatikana hadi maeneo ya vijijini.